CLICK TO VIEW ENGLISH TRANSLATION

Hivi karibuni Shirika la Children in Crossfire (CiC) limepata ruzuku kutoka taasisi ya Conrad N. Hilton Foundation ili kutekeleza mradi kabambe wa miaka mitatu (2021-2024) unaolenga kuchochea mchango bora wa asasi za kiraia katika harakati za kuleta matokeo chanya kupitia utekelezaji wa sera na mikakati ya kitaifa ya Malezi, Makuzi, na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM). Katika mradi huu uliopewa jina la ‘Mtoto Kwanza’ CiC itashirikiana na Mtandao wa MMMAM Tanzania (TECDEN) pamoja na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC).

Mradi huu wenye thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 3.4 utawezesha asasi za kiraia kutoa msaada mkubwa kwa Serikali ya Tanzania, ikiwa ni pamoja na mfumo mzima wa ushiriki wadau wa MMMAM hususan kwenye utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya MMMAM (PJT-MMMAM), ikiwemo uratibu wa kufuatilia matokeo ya utekelezaji wake kuanzia ngazi ya halmashauri hadi kitaifa.

Katika hotuba iliyosomwa na Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Doroth Gwajima wakati wa uzinduzi wa PJT-MMMAM uliofanyika Disemba 13, 2021, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Samia Suluhu Hassan alisema:

 

“Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ikitekelezwa kama ilivyopangwa italeta matokeo chanya katika ukuaji na maendeleo ya awali ya mtoto na kufikia maono mapana ya program hii ya kuwa: “Watoto wote nchini wanakua kwenye mwelekeo sahihi wa kufikia timilifu wao”.

“Watoto waliopata huduma za Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto watakuwa ni rasilimali watu wenye uwezo, ujuzi na wabunifu utakaowezesha kuongeza kwa uzalishaji na hivyo kuchangia kuimarisha uchumi wa familia na Taifa kwa ujumla katika siku za usoni katika kuimarisha Uchumi wa Kati ambao nchi yetu imeufikia.”

 

Naye Mtendaji Mkuu wa CiC, Richard Moore amesema:

 

“Kwa upande wetu tuna furaha kubwa kupokea msaada huu wa thamani sana kutoka Conrad N Hilton Foundation, taasisi ambayo ni kinara ulimwenguni kwenye Sekta ya MMMAM. Ninawashukuru kwa dhati kwa kutuamini. Ufadhili huu kwa Children in Crossfire ni uthibitisho tosha wa ubora wa kazi kubwa tunazofanya nchini Tanzania.

“Kwa takriban miaka kumi na tano sasa, Children in Crossfire imekuwa ikitekeleza miradi katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania, ikitoa fursa kwa maelfu ya watoto kupata elimu bora ya awali. Vilevile tumekuwa tukifanya kampeni ili mbinu zetu za kuboresha elimu ya awali zihawilishwe kwenye madarasa ya awali nchi nzima. Katika kipindi cha miaka mitatu ijayo, tutashirikiana katika kuratibu juhudi za kukuza utekelezaji wa shughuli za MMMAM Tanzania nzima. Uzoefu na utaalamu wetu utakuwa muhimu tunaposhirikiana na wadau wengine katika sekta ili kumpa kila mtoto wa Kitanzania mwanzo bora wa maisha, ikiwa ni pamoja na kupitia elimu.

“Ninatoa pongezi kwa wafanyakazi wetu na pia washirika wetu, ambao bila kuchoka, juhudi zao zimetufikisha katika hatua hii adhimu. Tuna shauku kubwa ya ukurasa unaofuata katika hadithi yetu hii na tuko tayari kukabili changamoto zozote zilizo mbele yetu.”

 

Peter Laugharn, Rais na Mtendaji Mkuu wa Conrad N. Hilton Foundation amesema:

 

“Dira ya Children in Crossfire ambayo ni ‘ulimwengu wenye huruma ambapo kila mtoto anaweza kufikia kiwango cha juu cha uwezo wake kamili’ inashabihiana vyema na maadili pamoja na mlengo wa taasisi yetu”.

“Moja ya malengo ya msingi ya mpango wa taasisi yetu kuhusu Malezi, Makuzi na Maendelao ya Awali ya Mtoto kimataifa ni kuhakikisha kuwa watoto wadogo wanakua kwa jinsi inavyostahiki. CiC imekuwa kinara kimataifa katika eneo hili nchini Tanzania kwa miaka mingi na ni mshirika wa serikali anayeheshimika. Tunatumaini kuwa ruzuku hii itasababisha kuongezeka kwa umakini na rasilimali zaidi kuwekezwa kwa watoto wadogo na hatimaye kuleta ufanisi endelevu katika mifumo inayosaidia ukuaji bora wa mtoto.”

 

Mradi huu utasaidia kujenga uwezo wa asasi za kiraia ili zishiriki kikamilifu katika mifumo ya ufuatiliaji kitaifa wa MMMAM, na pia kujenga mtandao wa asasi za kiraia kutoka mikoa yote 26 ya Tanzania Bara ili kushirikiana na serikali ngazi ya mikoa na halmashauri katika utekelezaji wa PJT-MMMAM.

Sauti za wanajamii zitapazwa zaidi kupitia mtandao wa waandishi mahiri wa habari za MMMAM wanaoripoti katika mikoa yote ya Tanzania Bara, ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa karibu na redio za jamii.