CLICK TO VIEW ENGLISH TRANSLATION

CHILDREN IN CROSSFIRE NA ECHIDNA GIVING WASHIRIKIANA KUBORESHA HUDUMA ZA MALEZI  NA ELIMU YA AWALI KWA WATOTO WADOGO KATIKA MAENEO YENYE MSONGAMANO MKUBWA WA WATU JIJINI DAR ES SALAAM

 

Children in Crossfire Tanzania ina furaha kubwa kutangaza ushirikiano wake mpya na taasisi ya kihisani ya Echidna Giving, unaolenga kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za malezi na elimu ya awali (ECE) kwa watoto wadogo katika baadhi ya maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu na kipato cha chini, jijini Dar es Salaam.

 

Ushirikiano huu wa kimkakati unaenda sambamba na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Tanzania 2050,  iliyozinduliwa hivi karibuni, ambayo inatoa kipaumbele kikubwa katika kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za malezi na elimu ya awali kwa usawa. Pia, utekelezaji wa afua mbalimbali katika mradi huu ni sehemu ya utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM), ambayo nayo inalenga kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata msingi imara wa ujifunzaji wa awali ili waweze kukua kwa utimilifu wao na kuwa na msingi bora katika ustawi wa maisha ya baadaye.

 

Kupitia ushirikiano huu wa miaka mitatu, Children in Crossfire, kwa msaada wa Echidna Giving, watapokea dola za Kimarekani 890,000 (sawa na takribani shilingi bilioni 2.3 za Kitanzania) ili kusaidia kuimarisha mifumo na kuchagiza mazingira wezeshi kwa vituo vya kulelea watoto wadogo mchana katika jiji la Dar es Salaam. Utekelezaji huo utafanyika kwa ushirikiano wa karibu na Umoja wa Wamiliki wa Vituo vya Kulelea Watoto Wadogo Mchana Dar es Salaam (UVIWADA).

 

Craig Ferla, Mkurugenzi Mkazi wa Children in Crossfire Tanzania, alisema:

“Msaada huu kutoka Echidna Giving unakuja katika wakati muhimu sana kwa Tanzania. Kadri nchi inavyopiga hatua kuelekea Dira ya Maendeleo 2050 ikiwa na kipaumbele cha kuhakikisha watoto wadogo wa Tanzania wanaendelezwa kufikia uwezo wao kamili, ufadhili huu utatusaidia kutimiza ahadi hiyo ya kitaifa—hasa kwa watoto wanaoishi katika jamii na maeneo ya mijini ambapo idadi ya watu inaongezeka kwa kasi kubwa.

“Tuna furaha kubwa kushirikiana kwa karibu na UVIWADA ili kuimarisha ubora na uendelevu wa vituo vya malezi, tukihakikisha watoto wadogo—hasa wasichana na watoto kutoka kaya zilizo na hali ya uhitaji sana—wanapata malezi bora na uchangamshi wanaohitaji katika miaka yao ya awali. Uwekezaji huu utachochea kuibua uwezo kamili wa watoto, kuuvunja mzunguko wa umasikini kwenye kaya wanakotoka Watoto hao, na hivyo kusaidia kufanikisha malengo makuu ya maendeleo ya taifa.”

 

Echidna Giving, ni mdau wa maendeleo anayetoa misaada. Taasisi hii inajulikana kimataifa katika kuendeleza elimu yenye usawa wa kijinsia. Kwa dhamira ya “kuhakikisha wasichana wengi zaidi wanapata elimu bora ili kuishi maisha bora”, taasisi hii imepanga kuwekeza hadi dola milioni 700 kwa kipindi cha miaka 40 ili kuhakikisha watoto katika nchi zenye kipato cha chini wanapata elimu bora inayozingatia usawa wa kijinsia.

 

Richard Moore, Mkurugenzi Mtendaji wa Children in Crossfire, aliongeza:

“Ushirikiano huu unaonyesha dhamira yetu ya dhati ya kusaidia watoto wadogo na wanaotoka kwenye kaya zenye kipato cha nchini Tanzania. Tunaishukuru Echidna Giving kwa kutambua ubora na uaminifu wa kazi yetu nchini Tanzania.

“Kwa kulenga malezi na elimu ya awali katika mazingira ya mijini yenye wakazi wengi wenye kipato cha chini, hatuchangii tu katika vipaumbele vya maendeleo ya taifa, bali pia tunawapa wasichana na wavulana fursa sawa ya kuanza Maisha kwa ubora ambao kila mtoto anastahili.”

Hatua hii mpya ya kuboresha Malezi ya Watoto wadogo, inajengwa juu ya juhudi endelevu za Children in Crossfire za kufanya huduma za malezi na elimu ya awali ziwe rahisi kufikiwa, shirikishi na zenye matokeo makubwa—hasa katika maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu,  na wenye wananchi wa kipato cha chini jijini Dar es Salaam. Kupitia msaada mkubwa wa Echidna Giving na ushirikiano na wadau wakuu wa kitaifa, mpango huu utaimarisha familia, kuwezesha jamii, na kusaidia kuweka msingi imara wa mustakabali wa Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Post comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.