CLICK TO VIEW ENGLISH TRANSLATION
TANZANIA YAANDAA WARSHA YA KIKANDA AFRIKA YA UFUNDISHAJI WA HISABATI, IKIZIKUTANISHA NCHI SABA KUJADILI MBINU ZENYE UFANISI DARASANI
Tanzania wiki hii ni mwenyeji wa warsha ya kikanda ya siku tano kuhusu Utafiti na Maendeleo ya Ufundishaji wa Hisabati (Numeracy Research and Development – NRD), inayowakutanisha maafisa wa serikali, wataalamu wa fani ya hisabati, viongozi wa programu na washirika wa utekelezaji kutoka nchi saba, kwa lengo la kubadilishana ushahidi na mbinu zinazotekelezeka za kuimarisha stadi za msingi za hisabati kwa watoto.
Warsha hiyo inafanyika Jijini Dodoma kuanzia 5 hadi 9 Oktoba 2026, ikiwa ni fursa kwa nchi zinazoshiriki kubadilishana uzoefu kuhusu mbinu zenye ufanisi darasani na kujadili namna mbinu hizo za ufundishaji wa hisabati za awali zinavyoweza kuimarishwa, kuendelezwa na kutekelezwa kwa kiwango kikubwa zaidi.
Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa warsha hiyo anatarajiwa kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, jambo linalodhihirisha dhamira ya Tanzania ya kuimarisha ujifunzaji wa stadi za msingi na kutambua nafasi muhimu ya serikali katika kuongoza na kuhakikisha maboresho ya ufundishaji wa hisabati yanaendelea na kufikia watoto wengi zaidi.
Programu ya NRD inalenga kuboresha ujifunzaji wa stadi za msingi kwa madarasa ya awali (Darasa la awali, Darasa la Kwanza hadi la Tatu), kupitia mbinu za ufundishaji zilizopangiliwa na zinazojumuisha mawanda na mtiririko wa ujifunzaji, mipango ya masomo, zana za ujifunzaji na ufundishaji wa umahiri wa kuhesabu kwa vitendo, tathmini pamoja na mafunzo kwa walimu. Warsha hiyo itaziwezesha timu/washiriki kutoka nchi zinazoshiriki kubadilishana uzoefu wa mbinu zilizojaribiwa na kuthibitishwa darasani, pamoja na kujenga mifumo endelevu inayotokana na ushahidi ambayo inaweza kuingizwa katika mifumo iliyopo ya elimu.
Mpango wa NRD, unatilia mkazo dhana kwamba “Stadi za hisabati ni msingi wa ujifunzaji mwingine wote,” alisema Tom Pugh, Mkurugenzi wa Programu ya NRD kutoka Genesis Analytics. “Mkutano huu unawakutanisha wataalamu na watekelezaji ili kuonesha mifumo inayofanya kazi kwa vitendo, ili mafanikio yanayopatikana katika wilaya moja yaweze kusambazwa na kuwa sehemu ya mifumo ya kitaifa.”
SERIKALI KUONGOZA TANGU MWANZO
Warsha itaanza siku ya Jumatatu kwa mapokezi rasmi kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikijumuisha ziara ya utambulisho wa wajumbe kutoka katika nchi zote saba zinazoshiriki. Maafisa wa Tanzania watawasilisha vipaumbele vya kitaifa katika kusoma, kuandika na kuhesabu kwa washiriki wote wa NRD. Baadaye, vikao vya majadiliano vitakavyofanyika mchana vitatoa fursa kwa serikali kutoka nchi mbalimbali kulinganisha uzoefu wao kuhusu mbinu za utekelezaji, upimaji wa matokeo na gharama, badala ya kupata taarifa kutoka kwa washirika wa programu pekee.
Kwa siku mbili Serikali itaongoza mada za warsha, utaratibu ambao umewekwa kwa makusudi ili serikali ioneshe msisitizo wake kwamba maboresho ya ufundishaji wa hisabati yana uwezekano mkubwa wa kufanikiwa pale ambapo serikali inamiliki mchakato huo, na hatimaye inakuwa na uwezo wa kuugharamia na kuutekeleza kwa kiwango kikubwa.
Kwa kuipa serikali nafasi ya kwanza kabla ya kuanza kwa vikao vya kitaalamu na vya ufundishaji, warsha inalenga kuhakikisha kuwa washirika wa utekelezaji wanazingatia mahitaji na vipaumbele halisi vya serikali, badala ya kujenga programu kwa kuzingatia matarajio ya wafadhili pekee.
Siku ya Ijumaa, wajumbe watasafiri kwenda Kondoa kwa ziara ya mafunzo, ikijumuisha mapokezi na utambulisho kutoka kwa uongozi wa Wilaya ya Kondoa, pamoja na kutembelea madarasa na kushuhudia moja kwa moja ujifunzaji na ufundishaji unavyotekelezwa darasani, na baadaye kufanya majadiliano na wadau wa elimu katika jamii ya Kondoa.
CHILDREN IN CROSSFIRE: MDAU MUHIMU KATIKA KUIMARISHA UFUNDISHAJI WA MSINGI WA HISABATI TANZANIA
Miongoni mwa washirika wa utekelezaji watakaowasilisha uzoefu wa darasani Dodoma ni shirika la Children in Crossfire, ambayo kazi yake ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa programu ya NRD nchini Tanzania.
Children in Crossfire ilichaguliwa kushiriki katika NRD kupitia mchakato wa ushindani uliowahusisha waombaji wengi, jambo linaloonesha uzoefu na uwezo wake wa kitaalamu katika eneo la ujifunzaji wa stadi za msingi nchini Tanzania.
Timu ya Children in Crossfire itashiriki katika vikao vya kitaalamu vinavyohusu ufundishaji wa hisabati katika madarasa mbalimbali, ikitoa uzoefu wa vitendo uliothibitishwa darasani kuhusu mbinu zinazoweza kuimarisha ufundishaji wa hisabati kwa watoto wa madarasa ya awali. Timu pia itachangia majadiliano kuhusu vifaa vya kufundishia na kujifunzia, ufuatiliaji wa utekelezaji darasani, na namna ya kuwasaidia walimu ili kuhakikisha ubora wa ufundishaji unaendelea hata pindi wigo wa programu utakapopanuliwa kwa kiwango kikubwa zaidi.
KUKUSANYA MBINU ZENYE UFANISI DARASANI
Kuanzia Jumanne hadi Alhamisi tarehe 6-8 Okt, warsha itajikita zaidi katika kile kinachotokea darasani.
Vikao vitakavyogawanywa kwa ngazi za madarasa vitawakutanisha wataalamu wa ufundishaji wa hisabati kutoka nchi mbalimbali barani Afrika kujadili kwa kina namna ufundishaji bora wa hisabati katika madarasa ya awali unavyopaswa kuwa.
Majadiliano yatahusisha namna watoto wanavyojenga uelewa wa dhana za hisabati kwa kutumia vifaa na vielelezo kama vile sehemu na jumla (part-part-whole), fremu za tano na kumi (five- and ten-frames), mstari wa namba na vifaa vya kuonesha thamani ya tarakimu kulingana na nafasi yake (place value).
Pia watajadili namna mipango ya masomo inavyoweza kuwasaidia walimu kueleza dhana za hisabati kwa uwazi na kwa mtiririko unaoeleweka, pamoja na namna ufuatiliaji, unasihi na jumuiya za kujifunza vya walimu zinavyoweza kusaidia kudumisha ubora wa ufundishaji baada ya mafunzo ya awali kukamilika.
Utengenezaji na usambazaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia, ufuatiliaji wa utekelezaji darasani na changamoto za kuwasaidia walimu kwa kiwango kikubwa pia vitajadiliwa kwa kuzingatia uzoefu wa nchi mbalimbali. Mshirika wa kitaalamu, taasisi ya Room to Read, atawasilisha mchango wake katika kuandaa na kusambaza vifaa vya ufundishaji vya NRD. Lengo ni kujenga maarifa hatua kwa hatua: ushahidi unaopatikana darasani kila siku, uzoefu wa wajumbe kutoka nchi mbalimbali na mbinu za kitaalamu vitakusanywa na kuendelezwa ili kujenga mkusanyiko wa pamoja wa mbinu zilizothibitishwa kuboresha ujifunzaji wa hisabati darasani.
Mbinu hizo zitakuwa zimejaribiwa na kuboreshwa katika mazingira ya nchi saba tofauti, badala ya kutengenezwa na kujaribiwa katika nchi moja pekee.
KUTOKA KWENYE USHAHIDI HADI UTEKELEZAJI KWA KIWANGO CHA KITAIFA
Warsha itahitimishwa kwa kurejea kwa msisitizo nafasi ya serikali, ikiwa ni hatua muhimu ya kuhakikisha maarifa na ushahidi uliopatikana vinaweza kutumika katika kuboresha mifumo ya kitaifa ya elimu. Vikao kuhusu kuimarisha ushirikiano na serikali na namna ya kubadilisha mafunzo ya warsha kuwa mipango ya utekelezaji ya kila nchi vinalenga kuunganisha moja kwa moja ushahidi wa darasani na maamuzi ya kisera na kifedha yanayohitajika ili mbinu bora ziweze kutumika kwa kiwango kikubwa.
Ujumbe wa kila nchi utabainisha maeneo ambayo wizara zinaweza kuhusishwa, ujumbe muhimu wa kitaalamu na ushahidi unaoweza kusaidia kujenga umiliki wa serikali bila kupunguza ubora wa programu. Kila nchi na programu itaondoka ikiwa na majukumu, ahadi na hatua zinazofuata zilizoainishwa kwa uwazi.
Mikakati inayojengwa wiki hii kati ya washirika wa utekelezaji na serikali inatarajiwa kuwa msingi wa kuwezesha programu zilizofanikiwa katika wilaya moja kuenezwa hadi wilaya nyingi na hatimaye kuwa sehemu ya programu za kitaifa.
Hatua hii ni muhimu pia katika kuhakikisha kuwa maboresho ya ufundishaji wa hisabati yanaweza kugharamiwa kwa muda mrefu. Mbinu zinazofanya kazi katika wilaya moja zinahitaji kuoneshwa kuwa zinaweza kufanya kazi na kugharamiwa kwa kiwango ambacho serikali inaweza kukidumisha kupitia bajeti zake, hata baada ya ufadhili kumalizika.
Pale warsha itakapohitimishwa, lengo si kuwa washiriki wamejifunza kutoka kwa kila mmoja pekee, bali serikali ziwe zimeondoka Dodoma zikiwa na uelewa mpana zaidi, unaotegemea ushahidi, kuhusu mbinu zinazostahili kuenezwa na kutekelezwa kitaifa. Aidha, washirika wa utekelezaji wanatarajiwa kuwa na uelewa mzuri zaidi wa namna ya kuwasilisha ushahidi na hoja zinazoweza kusaidia serikali kufanya maamuzi na kuchukua hatua.
KUHUSU NRD
Numeracy Research and Development (NRD) ni programu inayotekelezwa katika nchi saba kwa lengo la kuimarisha ufundishaji wa stadi za msingi za hisabati katika madarasa ya awali kupitia mfumo wa pamoja wa ufundishaji unaojumuisha uandaaji wa masomo, mafunzo kwa walimu, unasihi wa ufundishaji darasani na ufuatiliaji wa utekelezaji.
Programu hii inawakutanisha wizara za serikali, washirika watekelezaji, wataalamu na Gates Foundation kwa lengo la pamoja la kusaidia watoto kujenga stadi imara za msingi za hisabati kupitia mbinu za ufundishaji zilizothibitishwa kufanya kazi kwa ufanisi darasani.
NRD inafadhiliwa na Gates Foundation, Hempel Foundation pamoja na Founder’s Pledge.
Mawasiliano kwa Vyombo vya Habari:
Genesis Analytics: teminahm@genesis-analytics.com
Children in Crossfire: chiku.lweno@childrenincrossfire.org


