CLICK TO VIEW ENGLISH TRANSLATION
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Children in Crossfire, Richard Moore ametoa maelezo ya programu mpya ya miaka mitatu inayolenga maendeleo ya watoto ambapo amesema kuwa ‘itawapa mwanzo bora wa elimu zaidi ya watoto 11,000 wanaotoka kwenye familia zenye kipato cha chini.’
Programu hiyo ya Elimu ya Awali, inafadhiliwa na Taasisi ya Summerhill Foundation, yenye makao yake mjini Belfast, Ireland. Lengo la programu ni kuongeza ubora na upatikanaji wa Elimu ya Awali katika vituo 75 vya kulelea watoto wadogo mchana wanaotoka kwenye familia za hali ya chini, waishio kwenye maeneo yenye msongamano jijini Dar es Salaam.
Richard Moore amesema:
“Shirika la Children in Crossfire limekuwa likifanya kazi na kuchagiza mabadiliko ya kweli katika Elimu ya Awali katika maeneo ya vijijini nchini Tanzania kwa takriban miaka kumi na tano sasa. Tunafurahi kuwa, kutokana na ufadhili huu mpya na ushirikiano na Summerhill Foundation, tutaweza pia kuchochea kuleta matokeo chanya katika jamii za mjini.
“Vituo vya kulelea watoto wadogo mchana ambavyo nimewahi kuvitembelea mkoani Dar es Salaam hakika vinahitaji msaada wetu. Vituo vingi vina hali duni sana, vingine vina walimu ambao hawajapata mafunzo stahiki, madarasa hayana ubora, hakuna zana za kufundishia na kujifunzia zinazohitajika.
“Katika kipindi cha miaka mitatu ijayo, programu yetu itajikita katika kuandaa modeli ya umiliki wa vituo kijamii unaoweza kusaidia vituo hivi vya kulelea watoto mchana vitoe huduma bora ya Elimu ya Awali, hasa katika Malezi, Makuzi na Maedeleo ya Awali ya Mtoto, kusaidia uanzishwaji wa biashara yenye faida zaidi kupitia vituo hivyo, na kuinua kiwango cha utoaji wa Elimu ya Awali kwa ujumla, inayokidhi vigezo rasmi vilivyowekwa na serikali. Matokeo yake ni kuwa na watoto wanaokulia kwenye familia zenye kipato cha chini wanapata mwanzo mzuri wa elimu ambayo kila mtoto anastahili.
“Ninaishukuru sana Taasisi ya Summerhill kwa kuunga mkono kwa dhati shirika la Children in Crossfire ili liweze kushughulikia changamoto hii kubwa . Kwa pamoja tutaleta matokeo chanya ambayo yatadumu kwa miaka mingi ijayo, kubadilisha maisha ya maelfu ya watoto walio katika mazingira magumu kwa kupitia elimu.”
Jo Myles kutoka Summerhill Foundation aliongeza:
“Tunajivunia hatua yetu ya kuiunga mkono Children in Crossfire, shirika ambalo rekodi yake katika Elimu ya Awali ni ya kipekee kabisa. Programu hii mpya itabadilisha maisha ya watoto wengi wanaokabiliwa na umaskini katika jiji la Dar es Salaam, na kuwezesha mazingira bora ya maisha yao ya baadae.
Children in Crossfire ni shirika lisilo la kiserikali la kimataifa lenye makao yake makuu nchini Ireland ambalo madhumuni yake ni kutatua changamoto wanazopitia watoto wadogo wanaoishi kwenye umaskini na ukosefu wa haki mbali mbali ulimwenguni. Children in Crossfire Tanzania inalenga katika kuongeza upatikanaji huduma bora za Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali na kufungua fursa ili watoto waweze kufikia ukuaji timilifu.